Wakati Simba SC ikiwasili salama jijini Mbeya tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi Mbeya City, Wenyeji wametangaza kujihami kutokana na matokeo ya sare yanayowaandama.
Simba SC kesho Jumatano (Novemba 23) itakuwa Mgeni wa mchezo huo katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokione jijini Mbeya kuanza mishale ya saa kumi jioni.
Kocha Msaidizi wa Mbeya City Anthony Mwamlima amesema matokeo ya sare katika michezo ya nyuma wakiwa nyumbani yamewahuzunisha, lakini amewaahidi Mashabiki wao wanayafanyia kazi na kesho watakuwa tofauti.
Amesema wanakwenda kucheza na timu yenye uzoefu mkubwa katika Michezo ya Ligi Kuu na ile ya Kimataifa, hivyo wamejipanga kuikabili kwa hali zote, ili kuwafurahisha Mashabiki wao kwa matokeo yatakayowapa matokeo mazuri.
“Hatuna imani na haya matokeo ya sare tunayoyapata, Ligi ni ngumu na inatupasa kulinda nafasi yetu lakini unapopata sare mfululizo nyumbani haipendezi japo ni afadhali kuliko kupoteza.”
“Tunakwenda kukutana na Simba SC katika mchezo ambao tunauangalia kwa jicho la tatu, kwa sababu tunakwenda kukutana na timu kubwa ambayo ina uzoefu wa kutosha, na inacheza michezo ya Kimataifa, hivyo maandalizi yetu lazima yawe tofauti na tunavyojiandaa siku zote.” amesema Mwamlima
Mbeya City FC inakwenda kukutana na Simba SC ikikumbuka matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Geita Gold FC, huku Mnyama akikumbuka matokeo ya furaha mbele ya Ruvu Shooting iliyokubali kubugizwa mabao 4-0 mwishoni mwa Juma lililopita.