Kambi ya Timu ya Taifa ya Brazil imeingia hofu kubwa, kufuatia kuumia kwa Mshambuliaji Neymar da Silva Santos Júnior, akiwa katika mchezo wa Kwanza wa Kundi G dhidi ya Serbia, jana Alhamis (Novemba 24).
Neymar hakumaliza mchezo huo, kufuatia maumivu makali aliyoyatapa katika Kifundo cha Mguu wake wa Kulia, baada ya kuchezewa ndivyo sivyo na Nikola Milenkovic, hatua ambayo ilimfanya Kocha Mkuu wa Kikosi cha Brazil Adenor Leonardo Bacchi ‘Tite’ kumtoa nje.
Kocha Mkuu wa Brazil ‘Tite’ amesema Mshambuliaji huyo anatarajiwa kufanyiwa vipimo leo Ijumaa (Novemba 25), ili kufahamu ukubwa wa jeraha lake.
“Tunaimani Neymar ataendelea kuwa sehemu ya timu yetu, kesho (leo) atafanyiwa vipimo ili kufahamu ukubwa wa jeraha alilolipata,”
“Awali sikuona kama Neymar ameumia, lakini muda ulivyozidi kwenda niliona kuna mabadiliko, ndio maana niliamua kumtoa,” amesema kocha Tite.
Mshambuliaji huyo wa klabu ya Paris St-Germain, amekua akiandamwa na majeraha ya mara kwa mara, hususan katika mguu wake wa kulia.
Alikosa Fainali wa Copa Amerika mwaka 2019, kufuatia majeraha Kifundo cha Mguu wake wa Kulia, ambayo yalimlazimu kukaa nje kwa majuma kadhaa.
Brazil itacheza mchezo wa Pili wa Kundi G, Jumatatu (Novemba 28) dhidi ya Uswiz.