Rais wa Marekani, Joe Biden na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron wamesema wataiwajibisha Urusi kwa matendo yake nchini Ukraine, huku Umoja wa Ulaya ukitangaza ukomo wa bei ya mafuta ya Urusi, ili kuibania Moscow mapato ya kufadhili dhidi ya vita vyake Ukraine.
Biden pia amesema atakuwa tayari kuzungumza moja kwa moja na Rais wa Urusi Vladmir Putin kuhusu kumaliza vita, huku Putin akidai mara zote amekuwa tayari kwa mazungumzo, lakini matakwa ya Biden yatafanya mazungumzo hayo kutowezekana.
Mnamo Machi, mwezi mmoja baada ya kuanza kwa uvamizi wa Urusi, Biden alimuita Putin katili, kuhusiana na hatua zake na kusema kiongozi huyo wa Kremlin hawezi kusalia madarakani ambapo sasa anasema baada ya mkutano wake na Macron kwa pamoja na watasimama kidete dhidi ya ukatili wa Urusi.
Hata hivyo, ikiwa ni tayari miezi tisa baada ya mapigano na uwepo wa msimu wa baridi ukizidi, mataifa ya magharibi yanajaribu kuimarisha msaada wa Ukraine, wakati ikikabiliana na madhara ya mashambulizi ya makombora na droni yaliyowaacha mamilioni bila joto la majumbani, umeme na maji.