Washtakiwa watano akiwemo mama na watoto wake wawili wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya baba wa familia yao, Mange Washa (49) wamepandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya Kwimba na kusomewa shitaka la mauaji sambamba na watu wawili wanaodaiwa kulipwa Shilingi laki 8 na wanafamilia ili kutekeleza mauaji hayo .
Waliopandishwa kizimbani, katika kesi hiyo ya Jinai namba 12/2022 ni mke wa marehemu Hoka Mazuri (48),na watoto wake wawili ambao ni Masunga Mange na Paskali Mange huku wanaume hao wakiwa ni Shija Masalu (28) na Makoye Lusana (53), na kwa pamoja hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, Ndeko Dastan, Mwendesha mashtaka wa Serikali, Robert Mwanakatwe amesema Desemba Mosi 2022 washtakiwa walimuua Mange Washa kwa kumkata kichwa akiwa amelala nyumbani na kuomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine kutokana na upelelezi kutokukamilika.
Mara baada ya Mwendesha mashtaka kusoma ya maelezo hayo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama, Ndeko Dastan aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 28, 2022 itakapotajwa tena ambapo washtakiwa wanadaiwa kupanga njama na kumuuwa mwanaume huyo wakimtuhumu kuwanyima uhuru wa kutumia mali za nyumbani kwao.