Maafisa wa Umoja wa Mataifa, UN wamesema hadi sasa zaidi ya watu 160 wamefariki kutokana na mafuriko yaliyoukumba mji mkuu wa nchi ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, Kinshasa.
UN inasema, idadi hiyo imetolewa na mamlaka ya Serikali nchini DRC ambapo Mvua kubwa iliyonyesha siku ya Jumanne, ilisababisha mafuriko na barabara nyingi katikati mwa jiji la Kinshasa lenye watu wapatao milioni 15, zilijaa maji yaliyoathiri vibaya njia kuu inayoelekea kwenye bandari ya Matadi.
Aidha, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu pia imesema takriban nyumba 280 ziliharibiwa na mafuriko hayo na kutokana na vifo hivyo, Serikali litangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa.
Mafuriko hayo, yaliyoambatana na maporomoko ya udongo ndiyo yaliyopelekea vifo vingi na walio wengi ni watoto waliokufa baada ya nyumba nyingi kuanguka katika mtaa wa Binza Delvaux, uliopo kata ya Ngaliema jijini Kinshasa.