Mawaziri wa nishati wa Umoja wa Ulaya wameafikiana ukomo wa bei ya gesi asilia katika jumuiya hiyo, licha ya wasiwasi wa baadhi ya wanachama kuhusu namna sera hiyo inavyoweza kuathiri uwezo wa Ulaya wa kuvutia usambazaji wa gesi katika masoko ya kimataifa yenye ushindani wa bei.
Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya miezi kadhaa ya majadiliano ambapo Ulaya imekuwa ikishuhudia changamoto katika sekta ya nishati na hasa baada ya Urusi kukata usambazaji kufuatia vikwazo baada ya kuivamia Ukraine.
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov ameuita uamuzi huo kuwa ni shambulizi dhidi ya bei za soko na usiokubalika.
Kwa muda mrefu serikali ya Ujerumani imekuwa ikipinga hatua hiyo ikihofia athari za kiusambazaji ambazo ni pamoja na wauzaji wa gesi kugeukia masoko yenye bei za juu.