Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) limesema halijamzuia bondia Hassan Mwakinyo kupigana visiwani humo, lakini kuna taratibu ambazo promota wake ametakiwa kuzifuata.

Hivi karibuni kulikuwa na sintofahamu ya pambano hilo kuchezwa visiwani humo ikielezwa, Mwakinyo amezuiwa licha ya mchango wake kuhakikisha ngumi zinachezwa Zanzibar.

Katibu mtendaji wa BTMZ, Said Marine amesema si kweli kwamba wamezuia pambano hilo, lakini lilianza kutangzawa na promota kabla ya taratibu baadhi kukamilika.

“Pambano litafanyika, kuna masuala ilikuwa tunayaweka sawa ikiwamo kupata viongozi wa muda,” amesema

Mwakinyo atazichapa Mmarekani, Peter Dobson pambano la raundi 10 la uzani wa super welter la kuwania ubingwa wa WBC International, pambano ambalo lilikuwa na sintofahamu likielezwa kuzuiwa kuchezwa Zanzibar.

Japo Promota wa pambano hilo, Shomari Kimbau ameionyesha Mwananchi Digital barua ya ruhusa ya kuendelea na pambano ambayo imesainiwa na Abubakar Lunda na kugongwa mihuri ya BTMZ, Marine amesema bado kuna taratibu zinapaswa kufuatwa.

Barua hiyo ilieleza kwamba BTMZ inatoa idhini ya awali kwa kampuni ya Golden Boy African Promotion kuendelea na hatua muhimu za pambano hilo huku ikiitaka kusogeza mbele pambano hilo angalau kwa wiki mbili kutoka Desemba 30 iliyopangwa awali ili kutoa fursa kwa BTMZ kukamilisha mambo kadhaa.

Barua hiyo ilifafanua kwamba kufanikiwa kwa pambano hilo itaisaidia Zanzibar kuanza vema safari yake ya ngumi na kufafanua kwamba kwenye pambano hilo wapo mabondia kutoka visiwani humo pia watazichapa.

“Lunda ni msajili, atakuwa amefanya hivyo kwa upande wake, kwetu bado hatujatoa kibali, lakini narudia tena, BTMZ hatujazuia pambano la Mwakinyo kuchezwa, litafanyika kwa kuwa kuna vitu ambavyo inabidi tuviweke sawa ikiwamo kupata uongozi wa muda ambao utalisimamia

“Promota aliwahi kutangaza pambano hilo kabla ya kupewa kibali, lakini litakuwepo na litachezwa, wiki hii tutatangaza uongozi na taratibu zingine za pambano zitaendelea,” amesema Marine.

Promota wa pambano, Shomari Kimbau amesema wamelisogeza hadi Januari 12 ambapo litapigwa kwenye uwanja wa Mao se Tung, visiwani humo likitanguliwa na mengine 12.

Azam FC yang'ang'ana na Fei Toto
Ivan Toney anaswa tena sakata la KAMARI