Inaelezwa kuwa Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Senegal ‘Simba wa Teranga’ Aliou Cisse alikuwa anafikiria kuachana na timu hiyo, baada ya kutolewa katika Fainali za Kombe la Dunia 2020 nchini Qatar.
Senegal ilitolewa Hatua ya 16 Bora kwa kufungwa na England 3-0, baada ya kumaliza nafasi ya Pili kwenye Kundi A lililokuwa na timu za Uholanzi, Ecuador na Wenyeji Qatar.
Taarifa zinaeleza kuwa Cisse alifikiria kuchukua maamuzi ya kujiweka pembeni lakini alibadili mawazo na kuamua kuendelea na jukumu la kuwa Kocha wa Kikosi cha Taifa hilo la Afrika Magharibi.
Hata hivyo Inaeleza kuwa, baadhi ya Maafisa wa Shirikisho la Soka nchini Senegal wanavutana katika maamuzi ya kutaka kuondolewa kwa Kocha huyo, ili aajiriwe Kocha mwingine ambaye ataweza kuleta chachu ya kuifikisha mbali ‘Simba wa Teranga’.
Inaelezwa kuwa mjadala wa kufukuzwa ama kuachwa kwa Cisse umechukua nafasi kubwa ndani ya Shirikisho la Soka nchini Senegal, huku ikisemekana wakati wowote maamuzi rasmi yatatangazwa kuhusu hatma ya Kocha huyo, ambaye aliwahi kuitumikia Timu ya Taifa wakati wa Fainali za Kombe la Dunia 2002 zilizounguruma nchini Japan na Korea Kusini.
Kabla ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia kwa kuitoa Misri, Kocha Cisse alikiwezesha kikosi chake kutwaa Ubingwa wa Barani Afrika ‘AFCON 2021’ mapema mwaka huu katika Fainali zilizounguruma nchini Cameroon.
Senegal ilitwaa taji hilo kwa kuifunga Misri kwa changamoto ya Mikwaju ya Penati, baada ya kuwa na mchezo mzuri ndani ya dakika 120.