Uongozi wa Azam FC umesisitiza kuusubiri kwa hamu kubwa mchezo wa Mzunguuko wa 19 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans utakaopigwa jijini Dar es salaam.
Azam FC itakuwa mwenyeji wa mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Jumapili (Desemba 25) majira ya saa mbili usiku.
Kaimu Ofisa Habari wa Klabu hiyo Hasheem Ibwe amesema wapo tayari kwa mchezo huo, na wanaamini kikosi chao kitapambana ili kuzipata alama tatu muhimu. baada ya kuambulia alama mbili katika michezo ya Kanda ya Ziwa.
Ibwe ametoa kauli hiyo alipohojiwa na Kituo cha Radio cha EFM leo ijumaa (Desemba 23) ambapo amesema: “Kally Ongala na Benchi zima la ufundi lina hamu kubwa na huu mchezo wa Young Africans.”
“Tukishinda mechi hii tutakuwa tumerudi rasmi katika mbio za ubingwa. Tunajua ushindi utatufanya tupunguze gape ya pointi na wale walioko juu yetu. Tunaamini bado kuna mechi nyingi na huwezi kujua kitatokea kitu gani.”
“Kwetu Azam fc hatutotoa sare tena, ile sare na Geita Gold FC ndiyo ya mwisho kwa sasa ni ushindi tu. Tunatamani kushinda kila mchezo ulioko mbele yetu kwa sasa”