Kaimu Afisa Habari na Mawasilino wa Azam FC Hashim Ibwe ametuliza hali ya taharuki kwa Mashabiki wa Klabu hiyo kuhusu sakata la Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ ambalo lilishika hatamu mwishoni mwa juma lililopita.
Fei Toto aliandika ujumbe mzito katika ukurasa wake wa Instagram akiwaaga Mashabiki, Wanachama na Wachezaji wa Young Africans huku akihusishwa kujiunga na Azam FC.
Ibwe amesema taarifa za usajili wa Kiungo huyo kutua Azam FC alizisikia na kuziona katika Mitandao ya Kijamii, lakini hana jibu kamili kama ni kweli ama la.
Amesema suala hilo linapaswa kupewa muda, ambao kwa sasa unatoa nafasi kwa Klabu za Ligi Kuu kufanya usajili kuipitia Dirisha Dogo ambalo lilifunguliwa tangu Desemba 16, huku likitarajiwa kufungwa Januari 15-2023.
“Kwa sasa siwezi kuzungumzia suala la Fei Toto, japokuwa kuna mengi yanazungumzwa kuwa tunaweza kumsajili mchezo huyo na tumehusika kwa namna moja au nyingine kuondoka kwake katika Klabu ya Young Africans.”
“Muda ndio utakaoongea, baada ya muda kila kitu kitakuwa wazi kama ni kweli tumemsajili Feisal pamoja na wachezaji wengine tunaohusishwa nao” amesema Ibwe
Hata hivyo taarifa zisizo Rasmi zinaeleza kuwa, Feisal tayari amesharejea Kambini Young Africans kujiunga na wachezaji wenzake kwa ajili ya maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar.
Kiungo huyo alilazimika kuondolewa kwenye orodha ya Wachezaji waliocheza dhidi ya Azam FC juzi Jumapili (Desemba 25), kwa kile kilichoelezwa aliondoka kambini kabla ya kuanika wazi ujumbe mzito katika ukurasa wake wa Instagram.