Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Rais Samia ameelezeka kufanyika upya mapitio ya tathimini ya mradi wa ujenzi wa barabara hiyo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu kwa kuwa tathimini ya awali iliyofanyika mwaka 2018 imeonekana kupitwa na wakati.
Waziri Mbarawa ameyasema hayo hii leo Desemba 27, 2022 wakati akizungumza na wananchi wa mkoa wa Mbeya katika hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa barabara hizo na kutaja maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan juu ya mradi wa ujenzi wa Barabara ya Ibanda kuelekea Kajunjumele hadi Kiwira Port na Kajunjumele kuelekea Itungi Port.
Amesema Rais Samia ameelekeza utiaji saini wa mikataba hiyo ufanyike kwa kushuhudiwa na wananchi na si ofisini kama ilivyokuwa ikifanyika kwa miradi ya namna hiyo nyakati za nyuma na kwamba mradi huo ujengwe kwa teknolojia ya kisasa pamoja na kupatikana kwa mkandarasi mwenye viwango atakayeweza kuijenga barabara kwa teknolojia ya kisasa.
Aidha, Prof. Mbaraba pia ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya kutunza miundombinu ya barabara hizo ili ziweze kudumu muda mrefu na kumpa ushirikano mkandarasi ambaye anatakiwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.