Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka wananchi kujiunga na skimu mbalimbali za Bima ya Afya wakiwa na afya njema ili kuwa na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua.
Waziri Ummy, ameyasema hayo wakati wa ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, kuona hali ya utoaji huduma za afya na kusikiliza kero, ushauri na maoni ya wananchi juu ya upatikanaji wa huduma za afya.
Amesema “Matibabu sasa hivi ni gharama, ugonjwa ukija haukwambii nenda kakate Bima ya Afya kesho utaumwa, unaumwa tuu ghafla, tutatoa mwongozo wa gharama za kuchangia gharama za matibabu lakini ni vyema tukawa na Bima ya Afya.
Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kuweka utaratibu wa kutoa Bima ya Afya baada ya miezi mitatu toka kujiunga ili kudhibiti watu wenye nia ya kutaka kujiunga na Bima ya Afya mara baada ya kuumwa kwa kuwa kufanya hivyo kuna hatarisha uhai wa Mfuko wa Taifa wa Bima na Afya.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa huduma za Uzazi, Mama na Mtoto zitaendelea kutolewa bure katika Kliniki za ‘RCH’ na kuwataka watoa huduma kuzingatia maeleekezo ya Serikali na kutowatoza wananchi gharama kwa ajili ya huduma hizo.