Mchambuzi wa Soka la Bongo na Kimataifa Jemedari Said Kazumari ameibuka na kupinga maamuzi yaliyotangazwa na baadhi ya Wazee wa Klabu ya Young Africans jana Jumatano (Desemba 28).
Wazee wa Klabu hiyo Kongwe waliitisha Mkutano na Waandishi wa Habari na kueleza namna walivyosikitishwa na kitendo cha Kiungo Feisal Salum kutishia kuondoka Klabuni hapo, huku Azam FC ikitajwa kuhusika kwenye sakata hilo.
Wazee hao walikwenda mbali zaidi na kutangaza maazimio na kuwa tayari kutonunua tena bidhaa za Makampuni ya SSB (Said Salim Bakhresa) kwa kuonesha wamechukizwa na wanachodhaniwa kukifanya kwa Fei Toto, japo Uongozi wa Azam FC umekanusha kuhusiska na mpango huo.
Jemedari ameibuka leo Alhamis (Desemba 29) na kuandika ujumbe mzito katika Mitandao ya Kijamii na kuupa Kicha cha Habari kisemacho ‘HII NCHI INA WAJINGA WENGI SANA’.
“Kwani bado HAJAFIKA tu kambini AVIC TOWN? Si tunaambiwa ameomba na msamaha na KUKIRI kosa?
Nchi ya wajinga, ujinga umetamalaki, ujinga umeshika usukano na unaongoza njia, viongozi wa nchi ya wajinga wanatumia ujinga wa wananchi wao kama MTAJI katika kuficha madhaifu yao.
Nyakati hizi za kilo ya mchele 3,000 -3,500 (Afutatu , mpaka Afutatu miatano), maharage kilo 3,400 (Afutatu mianne) na vyakula vingine bei zikiwa zimepanda sana. Kuna ujinga wa kuambiana usinunue CHAKULA kwa yule kisa wamesajili mchezaji wetu.
Watu wenyewe tunakula TUNACHOKIONA sio TUNACHOKITAKA halafu tuongezewe na ujinga wa kuchagua anauza fulani usinunue. Ukiuliza kisa nini wamemchukua mchezaji wetu.
Wakati huo huo Uongozi wa Yanga umetuma barua ya kiofisi kuomba kusajili wachezaji 2 wa Azam FC. Huku kwenye nchi ya wajinga ambako ujinga umetamalaki tunaambiwa tusinunue bidhaa zao kisa kuna wajinga wenzetu wanasema Azam wanamtaka FEI.
Katika nchi ya wajinga pekeyake ndiko ambako wananchi tunaaminishwa mpira sio biashara mpaka pale sisi tunapotaka kununua au kuuza. Wenzetu wakitaka kwetu haikubaliki.
WAJINGA NDIO WALIWAO.
BIN KAZUMARI MTIPA (The voice of the voiceless)