Gwiji wa soka na mchezaji maarufu wa wa Mpira wa miguu Duniani, Mbrazil Edson Arantes do Nascimento maarufu kama Pele, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 82 kutokana na maradhi ya saratani.
Pele, aliiyeshi kwenye umaskini wa kutembea bila viatu hadi kuwa mmoja wa wanasoka wakubwa na mashuhuri wanaojulikana sana katika historia ya “Football”, alifariki dunia Alhamisi ya Desemba 29, 2022.
Kifo cha mwanasoka huyo pekee aliyeshinda Kombe la Dunia mara tatu, akiwa mchezaji wa time ya Taifa ya Brazil kilithibitishwa na binti yake, Kely Nascimento kupitia kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Pele, aiibeba Brazil kwenye kilele cha soka na kuwa balozi wa kimataifa wa mchezo huo katika safari iliyoanzia mitaa ya jimbo la Sao Paulo, ambapo alicheza mpira wa kutengenezwa na soksi iliyojaa magazeti au matambara, “Chandimu”.
Aliisaidia nchi yake kushinda Kombe la Dunia mwaka wa 1958, 1962 na 1970 na anabakia kuwa kinara wa ufungaji wa timu ya taifa akiwa amefunga mabao 77 katika mechi 92.
Pele pia alikuwa mfungaji mdogo zaidi wa Kombe la Dunia mwaka 1958 kwa kuifunga bao timu ya Wales akiwa na umri wa miaka 17, katika mashindano yaliyofanyika Stockholm, Sweden na hadi sasa bado ndiye mchezaji pekee chini ya miaka 18 kufunga bao katika Kombe la Dunia.