Klabu ya Young Africans imethibitisha kuwa itafanya usajili wa wachezaji wawili kabla ya kufungwa kwa Dirisha Dogo la Usajili, Januari 16.
Young Africans imekua ikisubiriwa kwa hamu kufanya usajili huo, baada ya kuhusishwa na majina kadhaa ya wachezaji ambao wamewahi kuwika na klabu za Soka nchini Tanzania na nje ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino wa Klabu hiyo inayoshikilia Taji la Tanzania Bara Ally Kamwe amesema, wamepanga kusajili Wachezaji wawili wa Kimataifa wa Kigeni wanaocheza nafasi za Ushambuliaji wa Kati na Beki wa Kati.
Ally Kamwe amesema katika eneo la Beki watasajili Mchezaji ambaye anashiriki kwenye Michuano ya Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ Mwezi huu ingawa hajamueka wazi.
Pia Ally Kamwe amekanusha Tetesi za Klabu hiyo kumuwinda Mshambuliaji wa zamani wa Wydad Casablanca Francy Kazadi, ambaye kwa sasa anawika na kikosi cha Singida Big Stars FC, katika Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023 inayoendelea Kisiwani Unguja ‘Zanzibar’.