Aliyekuwa kocha Mkuu wa muda wa Simba SC, Juma Mgunda ameshinda tuzo ya kocha bora wa mwezi Desemba wa ligi kuu ya NBC msimu wa 2022/23 na kuwashinda Nasreddine Nabi wa Yanga na Hans Pluijm wa Singida Big Stars alioingia nao hatua ya fainali.
Simba kwa matokeo ya mwezi huo ilipanda kutoka nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi hadi ya pili.
Mgunda aliiongoza Simba katika michezo mitano, ikishinda minne na kutoka sare mmoja, ambapo Simba ilizifunga: Coasta Union mabao 0-3, Geita Gold mabao 0-5, KMC mabao 1-3, Tanzania Prisons 7-1 na Kagera Sugar 1-1 (sare).
Kwa upande wa Nabi kwa mwezi huo aliongoza Yanga katika michezo minne kati ya sita ambayo timu hiyo ilicheza na kushinda yote, ambapo Yanga ilizifunga: Polisi Tanzania 3-0
Coastal Union 3-0, Azam FC 2-3 na Mtibwa Sugar 0-1.
Michezo mingine ambayo Yanga ilishinda mwezi huo, lakini Nabi hakuiongoza kutokana na kutumikia adhabu ni dhidi ya Prisons ambayo Yanga ilishinda bao 1- O na dhidi ya Namungo ambayo Yanga ilishinda mabao 0-2.
Pluijm kwa mwezi Desemba aliiongoza Singida katika michezo sita, akishinda minne, sare moja na kupoteza mmoja. Singida ilizifunga Namungo FC mabao 3- 0, Tanzania Prisons mabao 1-2, Dodoma Jiji bao 0-1 na Geita Gold mabao 2-1. Ilitoka sare ya bao moja na Mbeya City na ilifungwa na Coastal Union mabao 1-2.