Kocha Mkuu wa Mabingwa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Mohammed Nabi, ameshangazwa kuhusishwa na taarifa za kumkataa Kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye anakabiliwa na sakata la kujaribu kuvunja Mkataba klabuni hapo.

‘Fei Toto’ alijaribu kufanya hivyo Desemba 2022, lakini Kamati ya Sheria na Hadi za Wachezaji ya TFF imemuamuru kurudi Young Africans, kufuatia kujiridhisha mkataba wake na klabu hiyo upo halali kisheria.

Kocha Nabi amesema hakuwahi wala hatawahi kumkataa Kiungo huyo kwenye kikosi chake, kwa sababu anapendezwa na uwezo wake wa kupambana Uwanjani na kusaidia matokeo mazuri wanayoendelea kuyapata kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Amesema Fei Toto ni kama mwanawe wa kumzaa na alishutushwa sana kuona kilichokua kikiendelea kwenye Mitandao ya Kijamii, hasa baada ya kuandika ujumbe mzito wa kuwaaga Mashabiki na Wanachama wa Young Africans.

“Kuna watu wanaandika hapo mimi simtaki Feisal, mtoto wangu anafuatilia sana taarifa za mitandao, aliponiambia hili nilishtuka na baadaye nikamwambia labda wanamzungumzia Nabi mwingine sio mimi,”

“Feisal ni kijana wangu kama mchezaji mwingine, kiukweli ukiingia ndani ya moyo wangu naomba sana hili suala liishe haraka ili arejee ndani ya familia, naona makosa yake alivyochukua hatua ya kupigania maisha yake lakini ni mtoto wa familia anayetakiwa kusaidiwa na kuelimishwa”

“Huwezi kumtoa mtoto kwenye familia anapokosea, nafurahi kuona hata uongozi umetumia njia sahihi kutafuta haki yao, mimi kama kocha namhitaji kijana wangu na naomba haya yote yaishe haraka.” amesema Kocha Nasreddine Nabi

Baba wa Fei Toto afunguka safari ya CAS
Mo Dewji aibua shangwe Simba SC