Kocha wa Mkuu wa Young Africans Nasreddine Mohammed Nabi amefurahi na kuwapongeza viongozi wa klabu hiyo, kwa kufanikisha usajili wa kiungo kutoka Zanzibar Mudathir Yahya, ambaye amekiri alikuwa anamuhitaji kwa udi na uvumba.
Mudathir Yahya amesajiliwa Young Africans akiwa mchezaji huru wakati wa Dirisha Dogo la Usajili lililofungwa rasmi juzi Jumapili (Januari 15).
Kocha Nabi amesema Kiungo huyo wa zamani wa Azam FC, ana uwezo mkubwa ambao anaamini utakisaidia sana kikosi chake katika harakati za kutetea Ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu, pamoja na kufanya vizuri Kombe la Shirikisho Barani Afrika Hatua ya Makundi.
“Nimefurahi na nawapongeza viongozi wa Young Africans kwa kufanikisha usajili huu. Mudathir nilimuhitaji kwenye kikoso changu tangu msimu uliopita lakini haikuwa rahisi kumpata, ujio wake nimeufurahia.”
Akizungumzia kiwango alichoonyesha kwenye mchezo dhidi ya Ihefu FC Nabi amesema Mudathir amecheza kwa asilimia 50% ya vile anavyotaka acheze hivyo anaamini ataendelea kuimarika na atakapofikia asilimia 100% Mashabiki wa Young Africans watafurahi.
“Ninaamini bado hajaonesha uwezo wake kwa asilimia 100, amecheza vizuri dhidi ya Ihefu FC na mchango wake umeonekana kwa asilimia 50, ninaamini kuna siku mashabiki watafurahi zaidi ya leo (jana).” amesema Nabi
Mbali na Mudathir, wengine waliosajiliwa Young Africans wakati wa Dirisha Dogo ni Mlinda Lango Metacha Mnata, Beki Mamadou Doumbia (Mali) pamoja na Mshambuliaji Kennedy Musonda (Zambia).