Mlinda Lango wa Ihefu Fikirini Bakari ameelezea mazungumzo yake na kipa wa Yanga, Djigui Diara baada ya mchezo wao kumalizika jana Jumatatu kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Katika mchezo huo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 ikiwa ni kisasi dhidi ya wapinzani hao kwani katika mechi ya mzunguko wa kwanza Ihefu ikiwa nyumbani ilishinda 2-1.
Hata hivyo katika mpambano huo, Bakari alifanya makosa alipoudundisha mpira nje ya eneo lake bila kufahamu nyuma yake yupo mchezaji wa Yanga, Fiston Mayele.
Kipa huyo alijikuta akipokwa mpira huo na wakati akipambana na wenzake kuzuia hatari langoni baada ya piga nikupige, Mayele alikunjuka shuti zito na kwenda wavuni na kumuacha mchezaji huyo akilalama.
Baada ya mtanange huo kumalizika Diara alimfuata kipa huyo na kuzungumza kimyakimya kama ambavyo picha zimesambaa mitandaoni zikiwaonesha wawili hao.
“Alinifuata kweli na kubwa alinitia moyo kwamba makosa yapo kikawaida na humfanya mchezaji kuwa imara, hivyo nilipokea kwa mikono miwili ushauri wake,”
“Naamini haitajirudia na isitoshe ile nadundisha mpira kujiandaa kuupiga sikujua kama Mayele alikuwa nyuma kwa sababu mbele yangu niliona wachezaji wawili, hivyo nimejifunza kuwa makini dakika 90,” amesema kipa huyo.
Hata hivyo amewatoa hofu mashabiki na wadau wa soka mkoani Mbeya kuwa timu hiyo haitashuka daraja licha ya matokeo waliyonayo na kwamba mechi zilizobaki watashinda.
Chanzo: Mwanaspoti