Serikali nchini, imekemea tabia ya baadhi viongozi kuomba rushwa, ili kupitisha posho za madaraka kwa Walimu Wakuu na kutaka fedha zote zilipwe Benki katika akaunti ya Kiongozi husika.
Hayo yamebainishwa Mkoani Kagera hii leo Januari 19, 2023 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – (TAMISEMI), Angellah Kairuki na kuongeza kuwa watumishi wote wanatakiwa kuwa mfano bora kwa Taifa.
Waziri Kairuki, ameyasema hayo mkoani Kagera wakati alipokuwa akifungua kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa mkakati wa elimu na uwekaji wa mpango kazi kwa mwaka 2023, na kusema endapo Kiongozi yeyote atabainika kuwa na tabia hiyo atashughulikiwa.
Amesema, wapo baadhi ya Viongozi wa Elimu Mkoa na Wilaya ambao wamekuwa na tabia ya kuomba fedha (rushwa) kwa walimu wakuu wanapofuatilia vocha za malipo za posho ya madaraka kitu ambacho si sahihi na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja.