Nahodha wa timu ya Dodoma Jiji, Mbwana Kibacha amesema licha ya Simba SC kuwa na kikosi bora lakini wamejipanga kupata pointi tatu katika mchezo wa kesho, unaotarajiwa kupigwa saa 1 usiku, katika Uwanja wa Jamhuri jijini hapa.
Dodoma Jiji inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 21, huku Simba wakishika nafasi ya pili wakiwa na pointi 47.
Mchezo wa mzunguko wa kwanza, Simba SC iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Mkapa, bao la kujifunga la aliyekuwa beki wa Dodoma Jiji, Abdallah Shaibu ‘Ninja huku mengine yakifungwa na Habib Kyombo na Moses Phiri.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jumamosi (Januari 21) Kibacha amesema wanajua utakuwa mchezo mgumu lakini wamejiwekea malengo ya kupata pointi tatu.
“Tunacheza na timu ambayo ipo katika nafasi nzuri sisi kama wachezaji jukumu letu ni kucheza na kuhakikisha tunashinda.
“Tutahakikisha tunacheza vizuri kupata matokeo mazuri, tunawaheshimu Simba SC lakini lazima tupate ushindi,”amesema Kibacha.
Pia kocha msaidizi wa timu hiyo, Kassim Liyogope amesema wamejiandaa vizuri kisaikolojia na wachezaji wapo katika hali nzuri.
“Tunawoamba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi tuna kila sababu ya kupambana kupata pointi tatu kwa aina ya maandalizi ambayo tumeyafanya, naamini tutapata pointi tatu muhimu,” amesema kocha huyo.