Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Mahakama na mfumo wa utoaji haki, kuongeza juhudi katika kutatua changamoto mbalimbali, ikiwemo suala la Rushwa katika vyombo vya utoaji haki, pamoja na suala la upelelezi kuchukua muda mrefu.
Dkt. Mpango ameyasema hayo mara baada ya Matembezi ya Uzinduzi wa Wiki ya Sheria yaliofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere (Nyerere Square), Jijini Dodoma Januari 22, 2023 na kuwaasa wahusika katika mfumo wa utoaji wa haki kuendelea kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha huduma mbadala ya usuluhishi inapatikana na kufikika kwa urahisi.
Amesema, yamekuwepo malalamiko katika maeneo ya minada ya mifugo inayokamatwa kwenye hifadhi kuzuiwa au wahusika kutozwa faini ndogo, fedha za kigeni
zilizokamatwa mipakani kupotea mikononi mwa mahakama na hukumu kupindishwa ili kumpa ushindi mwenye fedha.
Aidha, Makamu wa Rais ametoa rai ya kushughulikiwa kwa malalamiko ya gharama kubwa za uendeshaji wa kesi na kulipia gharama za mawakili, hukumu kuandikwa kwa lugha ya kiingereza, watuhumiwa kukaa mahabusu muda mrefu kusubiri uchunguzi kukamilika pamoja na ukosefu wa elimu ya sheria kwa umma.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais pia ametoa wito kwa Mahakama kushirikiana vema na wadau katika kuimarisha utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi ili kuweza kufikia malengo yake kirahisi.
Amesema, mawakili wa kujitegemea wanapaswa kujielekeza katika kutoa elimu na ushauri sahihi kwa wateja wao kuhusu namna bora ya kutatua migogoro ikiwa ni pamoja na kutumia njia mbadala ya usuluhishi badala ya kuendelea na kesi mahakamani ambako watalipwa gharama kubwa zaidi za kuwatetea.
Aidha, ameziasa asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea kutoa elimu kwa umma, misaada kwa wananchi na kujenga uelewa kuhusu haki za msingi za kiraia na umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Dkt. Mpango pia ametoa wito kwa viongozi wa dini na viongozi wa mila kote nchini kuisadia Mahakama kuzungumza na wananchikuhusu umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.