Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Bima ya Afya kwa wote ni lazima ila hakuna kosa la kisheria wala hakuna mtanzania atakayekamatwa, kuwekwa ndani au kufungwa kwa kutokuwa na Bima hiyo licha ya kwamba ni muhimu.
Waziri Ummy ameyasema hayo na kuongeza kuwa asilimia 99 ya watu walio na Bima ya afya kwa hiari, karibu wote wamekata wakiwa wagonjwa na kusisitiza kuwa Bima hiyo ni muhimu kwani inamsaidia Mtanzania kupata huduma kwa urahisi.
Amesema, “Tumesema Bima ya Afya kwa wote ni lazima ila hakuna kosa la kisheria hapo, hakuna mtanzania atakamatwa, kuwekwa ndani au kufungwa kwa kukosa Bima ya Afya. Ila tunakwambia ukitaka kupata leseni ya biashara basi uwe na Bima ya Afya.”
Aidha, Waziri Ummy ameongeza kuwa, “Tuna kesi zenye ushahidi watanzania wanauza nyumba zao ili kugharamia matibabu ya mgonjwa, Bima ya Afya ni moja ya sehemu ya kumkomboa mwananchi maskini kwa sababu atapata huduma za matibabu bila ya kikwazo cha fedha.”