Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewateuwa viongozi mbalimbali akiwemo James Mwainyekule aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, imeeleza kuwa Rais Samia pia amemteua Janet Mbene kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), huku Rashid Mchatta akiwa Skauti Mkuu Tanzania akichukua nafasi ya Mwantumu Mahiza ambaye muda wake umemalizika.
Rais Samia pia amemteua Gilead Teri kuwa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), huku Damasi Mfugale akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), na pia kuwateua Makamishna wawawili wa Tume, akiwemo Caroline Mutahanamilwa anayekuwa Kamishna wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.
Mwingine ni Idd Mandi aliyeteuliwa kuwa Kamishna wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ambapo taarifa hiyo ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema uteuzi wa viongozi hao umeanza tarehe moja mwezi huu, (Februari mosi, 2023).