Uongozi wa KMC FC umekiri timu yao inapitia kipindi kigumu kufuatia michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayowakabili juma hili.
KMC FC itacheza dhidi ya Mabingwa watetezi Tanzania Bara Young Africans keshokutwa Jumatano (Februari 22), kisha itapapatuana na Azam FC Jumamosi (Februari 25) jijini Dar es salaam.
Afisa Habari wa KMC FC Christina Mwagala amesema kutokana na ratiba hiyo kikosi chao hakina budi kupambana, ili kupata alama sita zitakazowaweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu msimu huu.
Amesema ugumu watakaoupitia, pia unachangiwa na Presha ya wanaowakimbiza kwenye msimamo wa Ligi Kuu, pamoja na ushindani uliopo kwa sasa, lakini amesisitiza suala kubwa kwao ni kuhakikisha wanashinda na kufikia malengo waliojiwekea.
“Ukiangalia katika kipindi hiki, KMC FC inapitia wakati mgumu zaidi ya vipindi vyote, kwani Jumatano tunacheza na Young Africans kisha Jumamosi tunacheza na Azam FC ambayo inahitaji kujiweka vizuri, michezo yote ni migumu kwetu huku tukiwa katika nafasi ya 12 kwenye msimamo.”
“Ukiachana na michezo hiyo wanaotufuata nyuma wanapambana ili nao waweze kuja juu, lakini tumejipanga kufanya vizuri na hali ya kikosi ipo vizuri, wachezaji wetu ambao walikuwa majeruhi wamerejea kwa ajili ya kupambana ili kumaliza katika nafasi nzuri” amesema Mwagala
Kuhusu mchezo dhidi ya Young African Mwagala ameongeza: “Mchezo wetu dhidi ya Young Africans utakuwa mgumu kwa kuwa wao wapo katika Presha ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Mashindano mengine, pia wanaongoza kwenye msimamo, hivyo watahitaji matokeo mazuri.”
“Pia ukiangalia wamepishana alama sita na watani zao Simba SC, hivyo watahitaji ushindi ili wasipoteze alama kwa kupata alama tatu.”