Mshambuliaji kutoka nchini Zimbabwe Prince Dube amefichua siri ya kuiadhibu Simba SC katika michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu msimu huu 2022/23.

Dube aliifungia Azam FC bao la ushindi dhidi ya Simba SC katika mchezo wa Duru la kwanza mwezi Oktoba 2022, kisha akafanya hivyo kwa kufunga bao la mapema kwenye mpambano uliomalizika kwa sare ya 1-1, juzi Jumanne (Februari 21).

Dube amesema kitendo cha kuifunga Simba SC mfululizo msimu huu, kimechangiwa na ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka kwa watu wake wa karibu, ambao wamekuwa wakimrahisishia kazi yake Uwanjani.

Amesema ushirikiano kutoka kwa Wachezaji wenzake, Viongozi, Mashabiki na Familia yake umekuwa chanzo kikuu cha kufanikisha jukumu hilo, ambalo limeiwezesha Azam FC kuvuna alama nne kwa Simba SC msimu huu.

“Kuifunga Simba SC katika michezo miwili ni kwa sababu ya sapoti kutoka kwa wachezaji wenzangu, Uongozi, Familia yangu na Mashabiki wote kwa kunisapoti.” amesema Dube

Sare dhidi ya Simba SC imerejesha Azam FC katika nafasi ya tatu kwenye Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 44, sawa na Singida Big Stars iliyoshuka nafasi ya nne kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Wapeni watoto nafasi watimize ndoto zao: RC Telack
Serikali yafurahia utekelezaji miradi ya maendeleo