Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema watafanya msako katika kila nyumba na kuwachukulia hatua kali za kisheria wazazi na walezi wa wanafunzi 118 ambao hawajafika shuleni hadi sasa.
DC Ndemanga amesema wameandaa kikosi kazi ambacho kitapita kila nyumba kwa lengo la kuwasaka wanafunzi kidato cha kwanza ambao hawajafika shule mpaka sasa na watoro sugu.
”Watendaji wa kijiji na kata watashiriki katika kampeni ya kuwasaka watoto wa shule za msingi na sekondari ambao hawajaripoti shule na wale wasiofika shule”
Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Lindi, Rehema Nahale amesema sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mwamko mdogo wa wazazi kuhusu masuala ya elimu, upungufu wa walimu 214 wa shule za msingi na 111 shule za sekondari, umbali mrefu kutoka nyumbani kwenda shuleni na kurudi.
“Sisi kama idara ya elimu tuna jitahidi kutoa elimu kwa wazazi na wanafunzi waone umuhimu wa elimu,” amesema Rehama.
Nahale amesema mwaka wa masomo 2021 na 2022 wanafunzi 1,369 walisajiliwa kufanya mitihani ya upimaji wa majaribio kwenye shule 23 za sekondari kidato cha nne zilizosajiliwa, lakini wanafunzi 106 walifeli na wanafunzi 2855 kidato cha pili walifanya mtihani wa upimaji 89 walifeli.
Mzazi aliyejulikana kwa jina la Saidi Magega amesema wanajua umuhimu wa elimu lakini changamoto walikuwa nayo ni hali ngumu ya maisha kwani wanashindwa kupata mahitaji muhimu yanayotakiwa shuleni.