Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema Benchi la Ufundi limetumia muda mwingi kuongea na wachezaji, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi (Februari 25).

Simba SC itacheza ugenini Uwanja wa St Merry’s nchini Uganda dhidi ya wenyeji Vipers SC, katika mchezo wa Mzunguuko wanne wa Kundi C Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku ikitangulia kupoteza michezo miwili ya Kundi hilo dhidi ya Horoya AC na Raja Casablanca.

Kocha Robertinho amezungumza katika Mkutano maalum na Waandishi wa Habari nchini Uganda mapema leo Ijumaa (Februari 24), na kusema kikosi chake kimejiandaa vizuri kukabiliana na Vipers SC.

Amesema kubwa walichozungumza na wachezaji wao ni kuhusu mchezo huo, ambao timu yake inapaswa kushinda ili kufufua matumaini ya kuvuka Hatua ya Makundi na kutinga Robo Fainali.

“Mchezo wa kesho tunahitaji kuwa makini tukiwa na Mpira na tukiupoteza, tumewasisitiza wachezaji kwenye kutumia kila nafasi tutakayotengeneza, tunahitaji kupata pointi alama ugenini”

“Ninafahamu mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa kikosi cha wapinznai wetu, lakini hata Simba SC ina kikosi bora ambacho kina uwezo wa kupambana na kupata matokeo.”

“Yaliyotokea katika michezo iliyopita yameshapita na kubaki historia, dhumuni kubwa lililotuleta hapa Uganda ni kupata alama tatu, ili tuwe sehemu ya timu zitakazofikiriwa kuingia Robo Fainali.” amesema Robertinho

Kocha huyo kutoka nchini Brazil, kabla ya kujiriwa Simba SC mapema mwaka huu, alikuwa akikinoa kikosi cha Vipers SC na kukiwezesha kutwaa Ubingwa wa Uganda na Kombe la Shirikisho msimu uliopita 2021/22.

Onyango ashusha PRESHA Simba SC
Wanafunzi wasiofika shule kusakwa nyumba kwa nyumba