Imefahamika kuwa Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Uganda Vipers SC Roberto Luiz Bianch Pelliser, huenda akafungashiwa virago, endapo atapoteza mchezo wa leo Jumamosi (Februari 25) dhidi ya Simba SC.

Miamba hiyo ya Afrika Mashariki inakutaka kwenye mchezo huo wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ikiwa dhohofu’l hali, na hadi sasa inafuatana katika nafasi ya tatu na nne kwenye msimamo wa Kundi hilo.

Uongozi wa Vipers SC umetajwa kufanya kikao kizito na Kocha huyo kutoka nchini Brazil, na kumpa nafasi ya mwisho dhidi ya Simba SC, hivyo endapo atashindwa kuibuka na ushindi mkataba wake utavunjwa rasmi.

Uongozi wa Vipers SC umefikia hatua hiyo, baada ya matokeo mabovu, huku akiwa na Kocha Robeto Luiz akidaiwa kuwa na bifu na baadhi ya mabosi wake, kutokana na kukosoa sera za usajili za timu hiyo.

Kocha Roberto Luiz Bianch Pelliser aliajiriwa Vipers SC Desemba-2022, baada ya kuondoka kwa Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyeibukia Simba SC ya Tanzania.

Kabla ya kutua Vipers SC Kocha Roberto Luiz Bianch Pelliser , aliwahi kuvinoa vikosi vya klabu za Angola Petro de Luanda (2016–2019) na Interclube (2021), pia amewahi kuwa Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya nchi hiyo ‘Palancas Negras’ mwaka 2017.

Hadi sasa kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Vipers SC imejikusanyia alama moja baada ya kutoka sare ya 0-0 dhidi ya Horoya AC ya Guinea mwishoni mwa juma lililopita, huku Simba SC ikiambulia patupu na kujikuta ikiburuza mkia wa Kundi C.

Juuko Murshid atamba kuisasambua Simba SC
Mtibwa Sugar yatamba kushinda ugenini