Aliyekua Nahodha Msaidizi wa kikosi cha Liverpool Jamie Carragher anaamini Klabu ya Manchester City ilifanya makosa ya kuwauza baadhi ya wachezaji wake kwenye klabu ya Arsenal mwanzoni mwa msimu huu.
Arsenal FC imekuwa na mabadiliko makubwa msimu huu, kwani hadi sasa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya England, ikiwa na alama 60, ikifuatiwa na Manchester City yenye alama 55 huku Manchester United inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 49.
Carragher ambaye kwa sasa ni Mchambuzi wa Kituo cha televisheni cha SKY Sports cha England amesema, Biashara iliyofanyika baina ya klabu hizo, imekuwa chagizo kwa Arsenal kufanya vizuri.
Amesema wachezaji waliouzwa kutoka Manchester City kwenda Arsenal wana umri mdogo na wana kiu ya mafanikio, hivyo kinachotokea kwa sasa kinaakisi makosa ya Pep Guardiola.
“Manchester City hawatarudia kuwauzia Arsenal Wachezaji, Zinchenko kuuzwa Arsenal ilikuwa ni biashara ya kirafiki baina ya Pep Guardiola na Mikel Arteta, Pep alijua Arsenal watakuwa wakawaida tu hakujua anatengeneza Arsenal kuwa tishio kwake”
“Unapouza wachezaji wenye umri mdogo kama hawa, ni kama kamari, lakini kwangu ninaamini asilimia kubwa huwa wana uchu wa mafanikio na kudhihirisha ubora wao, hasa kama walikosa nafasi huko walikotoka.”
“Ni kosa kubwa sana limefanyika, lakini kumbuka kuna Biashara pia imefanyika, na Soka ni mchezo wa wazi na wenye ushindani kwa hiyo Arsenal wamepata walichokihitaji licha ya ushindani kuendelea katika Ligi ya England na hatujafahamu nani atakuwa Bingwa.” amesema Carragher
Mchezaji meingine aliyesajiliwa Arsenal akitokea Manchester City mwanzoni mwa msimu huu ni Gabriel Jesus ambaye hadi sasa ameshaifungia The Gunners mabao matano katika michezo kumi na nne aliocheza.