Nahodha na Mshambuliaji wa Vipers SC Milton Karisa amesema, yupo tayari kucheza soka nchini Tanzania, endapo atapata dili zuri mwishoni mwa msimu huu.
Karisa amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Vipers SC msimu huu 2022/23, tangu klabu hiyo ilipoanza kampeni ya kucheza Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Mshambuliaji huyo ambaye hakuongozana na Kikosi cha Vipers SC kilichocheza dhidi ya Simba SC jana Jumanne (Machi 07), amesema amekuwa akifuatilia Soka la Tanzania na kubaini lina muamko mkubwa.
Amesema watanzania wengi wanapenda Soka tofauti ya Uganda, ambako muamko unaendelea kufifia siku hadi siku, hali ambayo inapunguza ushindani katika Ligi yao.
“Napenda sana soka la Tanzania. Mashabiki wa huku wanapenda sana mpira. Wewe ulikuja Uganda na ukaona jinsi ilivyokuwa, huku mashabiki wana muamko zaidi na soka”
“Ni ndoto ya kila mchezaji kucheza sehemu yenye muamko wa mashabiki kama hapa Tanzania lakini zaidi ikija ofa nzuri mezani tutafanya kazi kwasababu tunahitaji kutengeneza pesa pia” amesema Karisa
Mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Simba SC uliopigwa nchini Uganda, Karisa hakumaliza kufuatia majeraha aliyoyapata kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika.