Mkuu wa mkoa wa Kagera, Albert Chalamila ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU, kufatilia na kufanya uchunguzi katika mradi wa kituo cha malori kilichojengwa kata ya Ijuganyondo manispaa ya Bukoba, kutokana na ujenzi huo kuwa na dosari ikiwemo taa zilizowekwa kuwa na mwanga hafifu.
Chalamila ameyasema hayo wakati alipofika kituoni hapo kuweka jiwe la msingi la mwendelezo wa ujenzi wa kituo hicho na kusema mara baada ya uchunguzi huo angependa kuona hatua stahiki zinafuatwa ili kujua uhalisia.
“Ukipita usiku hapa taa hizi ni sawa na kibatari kisicho na mafuta ya taa, kwahiyo natoa maelekezo kwamba taa hizi zinapaswa zibadirishwe. Maelekezo yangu ya pili TAKUKURU ifanye kazi ya kukagua mradi huu kwa ujumla ili kujua kama alituibia mkandarasi aweze kuwajibishwa vizuri” amesema Chalamila.
Kwa upande wake, Mkuu wa idara ya viwanda na biashara wa halmashauri ya manispaa ya Bukoba, Philbert Gozibeth amesema mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi milioni 475.5 hadi kukamilika kwake.