Rais Samia Suluhu Hassan amezitaka Klabu ya Simba SC na Young Africans kuendelea kufunga mabao kwenye michuano ya Kimataifa kwa sababu fedha zipo.
Rais Samia, ameazisha utaratibu wa kununua kila bao kwa Sh milioni 5 kwa michezo ya Kimataifa ya Simba inayoshiriki Ligi ya Mabingwa na Young Africans inayoshiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Rais alitoa kauli hiyo jana Jumapili (machi 19) jijini Dar es Salaam, alipohutubia kwenye hafla ya kumpongeza kutimiza miaka miwili madarakani iliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) kwenye Uwanja wa Uhuru.
“Nataka kuwahakikishia kuwa mama bado anazo, wekeni mipira kwenye wavu, jengeni jina la nchi bado zipo,” alisema Rais Samia akiwatoa hofu Simba na Yanga kuhusu fedha za motisha maarufu ‘Fedha za bao la mama.”
Pia alisema aliona utani kwenye mitandao ya kijamii kuwa anampigia Msigwa (Gerson, Msemaji Mkuu wa Serikali) amwambie mwamuzi amalize mpira (wakati wa mchezo wa Simba iliyoifunga Horoya ya Guinea mabao 7-0 juzi Jumamosi) maana fedha zimeisha na kusema kuwa si kweli bado fedha zipo.
Mpaka sasa Simba SC imeshachukua Sh milioni 45 na Young Africans imechukua Sh milioni 30 katika mabao waliyo funga tangu Rais Samia atoe ahadi hiyo Februari 14 mwaka huu.
Katika miaka miwili ya utawala wake, Rais Samia amefanya mambo makubwa kwenye michezo, utamaduni na sanaa na sekta hizi zilikuwa hazipewi kipaumbele hali iliyowafanya wasanii na wanamichezo kuonekana wana maisha duni lakini sasa sekta hizo zinachangia pato la taifa.
Sekta ya michezo imechangia zaidi ya Sh bilioni 1.7 katika pato la Taifa na serikali na imeendelea kujipanga kuhakikisha mchango wake unafikisha Sh bilioni 3 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Kwenye sanaa nchi imetangazwa vizuri na wasanii wengi kutoka ndani ya nchi na kwenye michezo Tanzania imepata heshima kwa kuwa na timu za michezo mbalimbali zikifanya vizuri ndani na nje ya nchi.
Rais Samia ndiye mdhamini wa mashindano ya Cecafa ya Ligi ya Wanawake kwa Dola za Marekani 100,000 (sawa na Sh 233,150,000) na kufanya kuitwa Cecafa Samia Cup.
Rais Samia anakuwa Rais wa pili kutoka Afrika Mashariki kudhamini Soka akitanguliwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambaye anadhamini mashindano ya wanaume ya Kombe la Kagame tangu mwaka 2002.
Pia michezo kama soka imefanya vizuri ambapo Serengeti Girls imeshiriki Kombe la Dunia na kufika Robo Fainali na Simba Queens imeshiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na kushika nafasi ya nne na Tembo Warriors kufika robo fainali kwenye mashandano ya Kombe la Dunia kwa Walemavu.
Aidha zimeanzishwa tuzo za muziki, tuzo za filamu, Mfuko wa Maendeleo ya Michezo, mashindano ya Samia Taifa Cup yanayoshirikisha mikoa yote, matamasha ya utamaduni na mchakato wa ujenzi wa Sports Arena katika eneo la Kawe, Dar es salaam.