Majogoo wa Jiji ‘Liverpool’ wameanza mchakato wa kumfukuzia beki anayekipiga SL Benfica ya Ureno, Antonio Silva huku taarifa zikiripoti meneja wa Klabu hiyo ya Alfield Jurgen Klopp anamuhitaji mchezaji huyo kwa udi na uvumba.
Ka mujibu wa mwaandishi wa habari wa GIVEMESPORT, Dean Jones, beki huyo ni chaguo la kwanza la Klopp katika usajili wa mwishoni mwa msimu huu.
Beki huyo wa Kimataifa wa Ureno amekiwasha msimu huu katika Ligi ya ndani na michuano ya Barani Ulaya, Liverpool inaifukuzia saini yake baada ya kuridhishwa na kiwango chake.
Akizungumza kupitia kituo cha televisheni, mwandishi huyo amesema: “Liverpool inataka saini ya Silva mwenye umri wa miaka 19, imeanza mipango ya kusuka kikosi baada ya kuboronga msimu huu,”
Aidha Liverpool itatakiwa itoe kiasi cha Pauni Milioni 88 ambayo iko katika kipengele cha mkataba wake ili imsajili kinda huyo kipindi cha usajili wa dirisha la kiangazi.
Wakati huohuo, Mshambuliaji Roberto Firmino ataondoka mwishoni mwa msimu huu baada ya mkataba wake kumalizika na kwa mujibu wa taarifa mabosi wa Liverpool wataingia sokoni kusaka mbadala wa mchezaji huyo.
Wachezaji wengine wa Liverpool ambao wapo mbioni kuondoka ni Naby Keita, Joel Matip, Nat Phillips, Fabinho, Alex Oxlade-Chamberlain, James Milner na Arthur Melo.
Liverpool imejikita nafasi ya sita ikiwa na alama 42 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, na itakuwa na kibarua kizito dhidi ya Manchester City mwishoni mwa juma lijalo.
Kwa sasa Liverpool inasaka nafasi ya kufuzu michuano ya Ligi Mabingwa Ulaya msimu ujao 2023/24, baada ya kupoteza mwelekeo.