Kocha Mkuu wa Maafande wa Ruvu Shooting Mbwana Makata amesema wachezaji wake wamekuwa katika maandalizi kambabe katika kipindi chote cha mapumziko ya Ligi Kuu, ili kufanikisha malengo ya kushinda michezo iliyosalia msimu huu 2022/23.

Ligi Kuu Tanzania Bara ilisimama ili kupisha michezo ya Kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’, huku Tanzania ikicheza dhidi ya Uganda mchezo wa nyumbani na ugenini.

Ruvu Shooting ambayo ipo nafasi ya 15 ikiwa na alama 20, imeweka kambi yake jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa, Aprili 9 kwenye Uwanja wa Sokoine.

Katika mchezo uliopita Maafande hao wakicheza kwenye uwanja huo waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City huku wakionesha soka safi na la kasi mwanzo mwisho.

Kocha Makatta amesema licha ya mapumziko kuyatumia kurekebisha makosa, lakini pia imewapunguzia kasi waliyokuwa nayo na sasa ni kama wanaanza upya kusuka nyota wake.

Amesema hadi sasa anaona bado kazi kubwa ipo kwa Mabeki na Washambuliaji wake, akieleza anaendelea kupambana na maeneo hayo kuhakikisha mchezo ujao wanaendeleza ushindi.

“Uliona mchezo uliopita tulicheza vizuri na kupata ushindi, lakini mapumziko haya vijana walienda kupumzika inamaana ile kasi imepungua tunaanza upya.”

“Tatizo kubwa lipo kwenye eneo la ulinzi na ushambuliaji kwa sababu katika michezo ya kirafiki tumeruhusu mabao mengi na kufunga machache, lazima nilifanyie kazi kabla ya mchezo ujao wa Ligi Kuu,” amesema Makatta.

Naye Mshambuliaji wa Ruvu Shooting Evaligestus Mujwahuki amesema, licha ya matumaini waliyonayo kuinusuru timu hiyo, lakini presha ni kubwa kikosini kutokana na kiu waliyonayo ya uhitaji wa alama tatu kwenye michezo iliyosalia. “Michezo iliyosalia tunafikiria ushindi ili kukwepa kushuka daraja, hatujakata tamaa,” amesema.

Nagelsmann aziingiza vitani Chelsea, Tottenham
Rais Mwinyi, Balozi Concar wateta ujenzi uwanja wa Ndege