Kikosi cha Namungo FC kimerejea mazoezini kuiwinda Mbeya City watakaokutana nayo Aprili 09 kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Dennis Kitambi akisema ana kazi ya kuiimarisha safu yake ya ulinzi.
Kocha Mkuu wa Namungo FC Denis Kitambi amesema changamoto waliyonayo kwa sasa ni kwenye safu ya ulinzi kwani imekuwa ikiruhusu mabao katika michezo ya hivi karibuni.
Katika michezo minne ilizopita, Namungo FC imeruhusu kufungwa mabao saba, ikichapwa na Young Africans mabao 2-0, ikafungwa na Kagera bao 1-0, iliifunga Geita Gold mabao 2-1 na ikatandikwa na Tanzania Prisons mabao 3-2.
Kocha Kitambi amesema wanahitaji kuifanyia marekebisho safu yao ya ulinzi ili wamalize vizuri michezo yao mitano ya ligi iliyobaki msimu huu.
“Tumerudi mazoezini na kubwa tunaloliangalia ni hilo ili kwa sababu katika michezo mitatu iliyopita tumeruhusu mabao mengi.”
“Sasa tunataka kuhakikisha michezo yetu iliyobaki tunakuwa vizuri na kupunguza makosa katika eneo hilo,” amesema Kitambi.
Amesema wanapambana ili kupata michezo ya kirafiki kabla ya kumalizika juma hili ili iwape mazoezi mazuri kuelekea mchezo wao dhidi Mbeya City.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliofanyika Novemba 4, mwaka jana kwenye Uwanja wa Sokoine, Namungo ililala kwa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City.
Namungo iko nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 32 ikifunga mabao 23 imefungwa 28.