Baada ya kufanikiwa kufuzu Robo Fainali kwa kuongoza msimamo wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans huenda wakakutana na mmoja wa miamba watatu kutoka ukanda wa Afrika Kaskazini au Magharibi.
Young Africans ilijihakikishia kumaliza nafasi ya kwanza katika msimamo wa Kundi D, baada ya kuichapa TP Mazembe 1-0 katika Uwanjani wa TP Mazembe mjini Lubumbashi jana Jumapili (April 02).
Kikanuni Mshindi wa kwanza wa kila kundi atakutana na mshindi wa pili wa makundi mengine, hivyo kumalizika kwa michezo ya Hatua ya Makundi jana Jumapili (April 02), kumetoa nafasi ya kila timu shiriki katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kufahamu anaweza kukutana na nani.
Young Africans inaweza kukutana na Rivers United ya Nigeria, Pyramids ya Misri au USM Alger ya Algeria, ambazo zimemaliza katika nafasi ya pili katika makundi A, B na C.
Hata hivyo timu hizo zinapaswa kusubiri hadi keshokutwa Jumatano (April 05), ambapo Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ litachezesha Droo ya Robo Fainali ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho mjini Cairo Misri.
Wakati Young Africans ikisubiri Droo ya Robo Fainali, ndugu zao Simba SC nao wanasubiri Droo kama hiyo upande wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika huku ikitarajia kupangwa aidha na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Esperance de Tunis ya Tunisia na Wydad Casablanca ya Morocco.
Simba SC imemaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, hivyo kikanuni inapangwa na moja ya timu zilizomaliza nafasi ya kwanza katika Kundi A, B na D.