Kikosi cha Ihefu FC kimejinasibu kuwa tayari kwa mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ utakaowakutanisha na Simba SC Ijumaa (April 07) katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Kocha wa msaidizi wa Ihefu, Zubery Katwila amesema wamejipanga vizuri kuelekea katika mchezo huo, na wana matumaini makubwa ya kupata ushindi mbele ya Simba SC, iliyorejea jana Jumapili (April 02), ikitokea Morocco ilipokuwa ikicheza mchezo wa mwisho wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Raja Casablanca.
“Vijana wapo vizuri na tunaendelea na mazoezi ya mwisho kabla ya kuivaa Simba SC kwenye mchezo huo wa robo fainali utakaochezwa Ijumaa.”
“Upande wetu tumejiandaa vizuri na tunaamini tutakuwa na matokeo mazuri ambayo yanamfanya kila mmoja afurahie kwa kile ambacho kitaonekana uwanjani,” amesema Katwila.
Kocha huyo ameongeza walikuwa na hali mbaya mwanzo kwenye msimu lakini sasa timu inafanya kile ambacho Benchi la Ufundi inahitaji baada ya maboresho makubwa yaliyofanywa wakati wa Dirisha Dogo la Usajili.
Mbali na mchezo huo wa Robo Fainali Ihefu FC itakutana tena na Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara juma Lijalo katika Uwanja wa Highland Estates, Mbarali mkoani Mbeya, baadaye itakipiga na Geita kwenye uwanja huo huo.
Ihefu imeweka rekodi ya kuwa mbabe wa vigogo katika Michezo ya Ligi Kuu inapocheza nyumbani kwake, kwa kuzisambaratisha Young Africans na Azam FC.
Tangu Ihefu FC ipoteze mchezo wa Ligi Kuu, Januari 16 dhidi ya Young Africans, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, imecheza michezo sita, mitano ikiwa ya Ligi na mmoja wa ASFC na imefanikiwa kushinda michezo mitano na saremoja (1-1) dhidi ya Singida.
Katika hatua ya 16 ya ASFC Ihefu iliisambaratisha Pan African kwa mabao 2-0 wakati hatua ya 32 iliichapa Namungo kwa mikwaju ya Penati 3-4 baada ya dakika 90 kumalika kwa suluhu.
Mshindi kati ya Simba SC na Ihefu itakutana na mshindi kati ya Mtibwa na Azam FC katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.