Timu ya Taifa ya Riadha ya Wavulana na Wasichana wenye umri chini ya miaka 18 na 20, imeingia kambini kujiandaa na mashindano ya Afrika.

Michuano ya Afrika inatarajiwa kufanyika kuanzia Aprili 27 hadi Mei 3, mwaka huu jijini Lusaka, Zambia.

Katika mashindano hayo, Tanzania itawakilishwa na Wanariadha 18 wakurusha Tufe, Sahani na Mkuki.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania ‘RT’ William Kallaghe amesema, timu hiyo imeingia kambini tangu jana Jumapili (April 02) baada ya kufanyika majaribio na mchujo wa kupata wachezaji wenye viwango bora.

“Tumepata timu imara ambayo naaimini itapeperusha vyema bendera ya Tanzania, timu imeanza mazoezi na nina imani itafanya vizuri,” amesema.

Amesema katika timu hiyo, Tanzania itawakilishwa na mwanariadha mahiri kutoka Zanzibar, MwanaAmina Hassan Mkwayu, anayerusha mkuki kwa ustadi mkubwa.

Kocha wa timu hiyo, Asha Abdallah, amesema kikosi kipo katika hali nzuri na anajivunia kuwa na timu imara ambayo anaamini itafanya vyema.

Kocha huyo amesema maandalizi yanaendelea na ana uhakika wa Tanzania kuvuna medali katika mashindano.

Mwanariadha, MwanaAmina amesema pamoja na mchezo wa kurusha mkuki kusahaulika nchini, atahakikisha anafanya vizuri na kutoa hamasa kwa vijana wengine kujitokeza kucheza na kuongeza idadi ya wanamichezo wa kurusha mkuki.

“Hii itakuwa mara yangu ya kwanza kushiriki mashindano ya kimataifa, ninaendelea kujipanga vyema na nina uhakika nitafanya vizuri,” amesema.

Timu ya wachezaji wenye umri wa miaka 18 na mita wanazokimbia katika mabano inaundwa na Said Hamad Ali na Alex Sezari (mita 100), Nicodemus Joseph (mita 1500/5000) wakati Nasra Abdallah na Siwema Julius (mita 1000) huku Nasra Abdallah na Berthet Everist wakikimbia mita 200.

Wanariadha wenye umri chini ya miaka 20 ni Gasis Geagase Girihuda, Elia Clement na Said Ali (mita 100), Elia Clement Benedicto Martius na Gasis Geagase Girihuda (mita 200).

Wengine watakaorusha tufe, sahani na mkuki ni Mpaji Gipso, Samir Mbaraka Sururu, Hafidh Talib na Mwanaamina.

Robertinho azitumia salamu Ihefu FC, Young Africans
Guardiola: Vijana wamenifurahisha sana