Meneja wa Majogoo wa Jiji ‘Liverpool’ Jurgen Klopp amesema kipigo cha mabao 4-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi Manchester City uliopigwa Uwanja wa Etihad juzi Jumamosi (April Mosi), hakikubaliki.
Liverpool ilifunga bao la kuongoza kupitia kwa Mohamed Salah katika dakika ya 17, lakini Julian Alvarez alisawazisha dakika 10 baadae kabla Kevin de Bruyne, Ilkay Gundogan na Jack Grealish hawajaongeza mabao mengine na kuondoka na ushindi mnono.
Klopp amesema timu yake imekuwa ikicheza chini ya kiwango mara kwa mara msimu huu, hali ainayopelekea kupokea matokeo mabaya mabayo hayafurahishi klabuni hapo.
“Kuruhusu kufungwa mabao mawili ya haraka haraka kuliharibu kila kitu,” Klopp aliiambia BBC Sport.
“Jinsi tulivyoruhusu mabao, haikubaliki, tulishindwa kabisa, haikubaliki.”
“City walitawala mpira kila idara baada ya hapo na walikuwa na uwezo wa kufanya lolote walilotaka.”
“Tuna bahati hawakuwa vizuri, vinginevyo ingekuwa maafa zaidi.”
Kufautia kipigo hicho Liverpool iko nyuma kwa tofauti ya alama saba dhidi ya mbio za kuwania nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa ikiwa nafasi ya nane na beki wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand amesema, “ni wakati wa kuogopa kwa Reds”.
Mshambuliaji wa zamani wa England, Alan Shearer aliiambia BBC Match of the Day: “Liverpool ilikuwa mbali, haikuwa na kitu leo (juzi)”.
Kipigo hicho kwa Liverpool ni cha tisa kwenye Ligi Kuu msimu wa mwaka 2022-23 na wako nafasi ya nane kwenye msimamo, ikiwa ni mwenendo mbaya ndani ya msimu tangu msimu wa mwaka 2014-15.
Msimu uliopita Liverpool ilikuwa vizuri na kukosa ubingwa siku ya mwisho kwa tofauti ya alama moja dhidi ya City na kupoteza mchezo wa Fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Real Madrid, lakini kampeni za msimu huu hali imekuwa tofauti.