Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa nchini Tunisia Esperance de Tunis Nabil Maalou ameweka wazi hatapendezwa endapo klabu hiyo itapangwa kukutana na Simba SC ya Tanzania katika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ linatarajia kuchezeshwa Droo ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani humo keshokutwa Jumatano (April 05) mjini Cairo Misri, huku Simba SC iliyomaliza nafasi ya pili katika Kundi C, ikitarajiwa kupangwa aidha na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Esperance de Tunis ya Tunisia au Wydad Athletic Club ya Morocco.
Kocha Maalou amesema ikitokea kikosi chake kimepangwa na Simba SC hatokuwa mwenye amani sana katika ushindani wa mchezo huo, kwa sababu timu hiyo ya Tanzania imekua na matokeo ya ajabu inapokua nyumbani kwao Dar es salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Sababu nyingine iliyowekwa wazi na Kocha huyo kutoka nchini Tunisia ni umbali kutoka nchini kwao hadi Tanzania, akiamini hilo huenda likawachosha wachezaji wake kabla ya mchezo.
Amesema itapendeza kikosi chake kikipangwa na timu za Al Ahly au JS Kabylie ambazo anaamini ni afadhali kwa sababu zimekuwa zikicheza soka katika mazingira alioyazoea na zipo karibu nan chi ya Tunisia.
“Ninapendelea kupangwa na Al Ahly au JS Kabylie hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kwa sababu ya ukaribu wa nchi zinapotokea klabu hizo.”
“Sipendelei kupangwa na Simba SC kutokana na umbali kati ya Tanzania na Tunisia na mashabiki wao pia ambao wamekua wakichangia matokeo ya ajabu wanapocheza nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam.” amesema Kocha Maalou
Hata hivyo Simba SC haijawahi kukutana na Esperance de Tunis tangu ilipoanza kushiriki Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF, na ikitokea timu hizo zinapangwa kukutana Robo Fainali, itakua ni mara ya kwanza.
Esperance de Tunis imewahi kuja Tanzania kucheza dhidi ya Azam FC katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu wa 2016/17, ambapo katika mchezo wa Mkondo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Azam Copmplex Chamazi Azam FC ilichomoza na ushindi wa 2-1.
Matokeo hayo yaligeuka katika mchezo wa mkondo wa pili uliopigwa nchini Tunisia, ambapo Azam FC ilikubali kubanjuliwa mabao 3-0 na kung’olewa mashindanoni.
Simba SC imekua ikiishia hatua ya Robo Fainali tangu ilipochomoa makucha yake ya kupambana kwa nguvu kubwa Barani Afrika kuanzia msimu wa 2018/19, na msimu huu imedhamiria kufika Nusu Fainali ya Michuano hiyo ya CAF.