Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amezitaka Wizara, Taasisi za Umma, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekta Binafsi, Watanzania wanaoishi Ughaibuni (Diaspora) na Wadau wote wa maendeleo kutoa ushirikiano wa maoni na taarifa kwa timu ya Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ili uchambuzi uwe halisia na toshelevu.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Mchakato wa Maandalizi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma hii leo Aprili 3, 2023 na kuongeza kuwa, dira hiyo inatarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii ili kufikia lengo la kuwa Taifa lenye ustawi.

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango akiwakabidhi Waandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
Dkt. Suzan Mlawi na Prof. Samuel Wangwe muongozo wa maandalizi ya dira hiyo mara baada ya kuzindua Mchakato wa Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika hafla iliofanyika jijini Dodoma Aprili 3, 2023. Kulia ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba.

Amesema, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha katika maandalizi ya Dira hiyo, Watanzania kutoka pande zote za nchi, kutoka matabaka mbalimbali ya maisha, makundi mahsusi kama Bunge na Mahakama yatapata nafasi ya kuchangia mawazo yao ili kukuza tija katika sekta zote za uzalishaji na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa Upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 imeweza kufanikisha hatua mbalimbali za kimaendeleo kama vile uboreshaji wa miundombinu , ongezeko la shule, ukuaji wa sekta ya michezo pamoja na ukuaji wa uchumi kwa
wananchi na taifa kwa ujumla.

Awali, akitoa taarifa ya Mchakato wa Maandalizi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Natu Mwamba amesema chimbuko la Maandalizi ya Dira 2050 imetokana na kuendeleza mafanikio yaliofikiwa kutokana na utekelezaji wa Dira 2025 pamoja na uhitaji
wa mkakati utakaowezesha nchi kunufaika na maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia yanayoendelea kuibuka duniani.

Wanahabari wampa Mwendesha Mashitaka siku saba
Tanzania kushirikiana na WHO kanuni za Afya Kimataifa