Msemaji wa Serikali ya Burkina Faso amesema nchi hiyo imewatimua maripota wa magazeti ya Ufaransa ya ‘Le Monde’ na ‘Libération’ ikiwa ni muendelezo wa hatua za nchi hiyo Afrika Magharibi za kukabiliana na vyombo vya habari vya nchi hiyo ya Ulaya.

Amesema, wanahabari hao wamefukuzwa nchini humo kwa kuandika habari na makala za uwongo na upotoshaji ili kuichafua sura ya nchi. Maripota hao waliwasili Paris jana Jumapili, baada ya kutumiliwa nchini Burkina Faso juzi Jumamosi.

Hata hivyo uongozi wa gazeti la Kifaransa la Le Monde umesema katika taarifa kuwa, ”Ripota wetu nchini Burkina Faso, Sophie Douce amefukuzwa nchini humo, sawa na mwenzake wa gazeti la Libération, Agnes Faivre. Tunaalani hatua hiyo ambayo haihalalishiki kivyovyote.”

Toleo la Machi 27 la gazeti la ‘Libération’ lilichapisha habari ya upekuzi, iliyoonesha mauaji yaliyofanywa na eti na askari wa nchi hiyo, dhidi ya watoto na vijana mabarobaro katika kambi za kijeshi nchini humo. 

Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwezi uliopita, Burkina Faso ilisimamisha matangazo ya kanali ya televisheni ya Ufaransa ya France 24, baada ya chombo hicho kurusha hewani mahojiano kiliyoyafanya na kiongozi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda tawi la Kaskazini mwa Afrika AQIM.

Waziri wa Mawasiliano wa Burkina Faso Jean-Emmanuel Ouedraogo, alisema katika taarifa kuwa, “France 24 si tu imegeuka na kuwa msemaji wa hawa magaidi, lakini mbaya zaidi, imekuwa uwanja wa kuhalalisha vitendo vya kigaidi na matamshi ya chuki.”

Burkina Faso na mkoloni wake huyo wa zamani wa Ulaya zimekuwa zikivutana na kulumbana kwa miaka mingi sasa juu ya mambo mbali mbali. Mwezi uliopita, Burkina Faso ilivunja rasmi makubaliano ya kijeshi iliyosaini na Ufaransa mwaka 1961, wiki chache baada ya kumtaka mkoloni wake huyo wa zamani kuondoa vikosi vyake na balozi wake nchini humo.

Kocha PSG amtetea Lionel Messi
Farid Mussa: Nilitumwa kufanya nilichokifanya