Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain, Christophe Galtier amewajia juu mashabiki baada ya kumzomea staa wa timu hiyo, Lionel Messi huku wengine wakimpulizia filimbi.
Messi alizomewa baada ya PSG kufungwa bao 1-0 dhidi ya Lyon kwenye mchezo wa Ligue 1 uliyochezwa juzi Jumapili (April 02) ikichochea sintofahamu kuhusu mkataba wake.
Mashabiki hao hawakuvutiwa na kiwango cha Messi lakini kocha wa timu hiyo akamtetea akidai hata wachezaji wengine wana majukumu ya kuonyesha viwango bora.
Galtier amesema: “Kumpulizia filimbi Messi ni jambo la kushangaza, ni mchezaji aliyetoa mchango mkubwa kwenye timu, tangu msimu ulipoanza mchango wake umeonekana, lakini hata wachezaji wengine wasibweteke kwenye mechi.”
Mkataba wa Messi utakapomalizika mwishoni mwa msimu huku taarifa zikiripoti staa huyo anahusishwa na klabu yake ya zamani ya FC Barcelona.
Vilevile staa huyo wa kimataifa wa Argentina amehusishwa na timu kutoka Ligi Kuu Marekani maarufu ‘Major League Clubs (MLS).
Wakati hayo yakiendelea PSG inaendelea kumshawishi Messi mwenye umei wa miaka 35, asaini mkataba mpya hata hivyo mpaka sasa bado hajafanya uamuzi.
Juma lililopita FC Barcelona ilisema iko tayari kumrudisha Messi msimu utakapomalizika licha ya PSG kuweka mgomo. Taarifa ziliripoti FC Barcelona iliwasiliana na Messi.
Licha ya kichapo miamba hiyo kutoka Ufaransa inaendelea kuongoza ligi kwa alama 66 sita dhidi ya Lens ambayo inashika nafasi ya pili.