Aliyekuwa Beki wa FC Barcelona Gerard Pique ameuonya Uongozi wa Klabu hiyo kuhusu mpango wa kumrudisha Mshambuliaji wao wa zamani Lionel Messi, kwa kusema hakuna haja ya kufanya hivyo.
Messi anakaribia mwisho wa mkataba wake wa miaka miwili na Paris Saint Germain, baada ya kujiunga na wababe hao wa Ligue 1 wakati shida ya kifedha ilipomlazimu kuondoka Barca mwaka 2021.
Mustakabali wa mshindi huyo wa Kombe la Dunia haujulikani, huku Barca wakihusishwa mara kwa mara na kutaka kumsajili mfungaji bora wa muda wote, huku Inter Miami inayomilikiwa na David Beckham pia wakitaka kumvutia Ligi Kuu ya Mareakani, MLS.
Wakati Kocha Mkuu wa PSG, Christophe Galtier, akifichua kuwa klabu hiyo inapanga mazungumzo na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35, Makamu wa Rais wa Blaugrana, Rafael Yuste amekiri anapenda kumuona Mshambuliaji huyo akirejea Camp Nou.
Pique, ambaye alitangaza kustaafu soka mapema msimu huu, alishinda mataji nane ya La Liga na Messi akiwa Bárca, pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu na Klabu Bingwa Dunia mara tatu.
Lakini beki huyo wa zamani anasisitiza kwamba muunganiko unaowezekana kati ya klabu yake ya zamani na mchezaji mwenza lazima ufanyike kwa kawaida.
“Anamfahamu Yuste na ni mtu mzuri ambaye atakuambia kila wakati kile unachotaka kusikia,” Pique alisema wakati wa mahojiano na Gerardo Moreno. “Kulazimisha hali, kunaweza kutokuwa na tija”
“Mambo lazima yaende kawaida, ikibidi kufanywa, itafanyika. Wakati kuna nia ya pande zote mbili, operesheni katika soka inaweza kufanikiwa kila wakati.”