Baada ya kutolewa katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ kwa kufungwa 2-0 na Azam FC, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar Salum Shaban Mayanga, ametaja sababu za kichapo hicho kwa kuelekeza lawama kwa wachezaji wake.

Mtibwa Sugar iliangushiwa kisago hicho juzi Jumatatu (April 03) katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam, na kuondolewa katika Michuano hiyo ambayo Bingwa wake huiwakilisha Tanzania Katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Kocha Mayanga amesema Azam FC ilitumia udhaifu wa wachezaji wa Mtibwa Sugar kupata mabao ya ushindi, baada ya wachezaji wake kukosá umakini katika kila idara.

Amesema laiti kama wachezaji wake wangetumia nafasi ya upungufu wa mchezaji Daniel Amoah wa Azam FC aliyeonyeshwa kadi nyekundu, wangeweza kupata matokeo mazuri.

Hata hivyo, kocha huyo amesema timu yake itajipanga vizuri na kufanya vyema katika míchuano hiyo msimu ujao.

Kwa ushindi huo wa 2-0, Azam FC inaungana na Singida Big Stars iliyotangulia Nusu Fainali tangu Jumapili (April 02), baada ya kuisasambua Mbeya City FC katika Uwanja wa Liti mjini Singida.

Katika mchezo wa Nusu Fainali, Azam FC itaumana na mshindi kati ya Simba SC na Ihefu ambazo zitakutana katika mchezo wa Robo Fainali utakayopigwa keshokutwa Ijumaa (April 07) katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Singida Big Stars anamsubiri mshindi wa mchezo kati ya Young Africans na Geita Gold FC, ambao utapigwa Jumamosi (April 08), katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.

Jurgen Klopp agoma kuachia ngazi Liverpool
Wasiojulikana wateka Wanafunzi 10 Sekondari ya Umma