Mgonjwa mmoja kati ya watatu, ambao waliugua ugonjwa wa Marburg na kulazwa kwa matibabu katika Hospitali ya Bujunangoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba amepona na ameruhusiwa baada ya kukaa hosipitalini kwa muda wa siku 23.

Akizungumza na waandishi wa Habari Hospitali ya Bujunangoma baada ya kuruhusiwa, mtu huyo (jina limehifadhiwa), ameshukuru juhudi za Serikali kimatibabu licha ya kuwa amewapoteza wanafamilia wake akiwemo mama yake mzazi kwa ugonjwa huo wa Marburg.

Amesema, “Serikali ulivyotangaza huo ugonjwa, wakaja wakaniambia na mimi nina ugonjwa huo nilistuka kwakuwa nilipata taarifa, maana huu ugonjwa ulimuua mama yangu, ukaua Shangazi, ukaua na mtoto wa shangazi yangu na nikawa siamini kama nitapona.”

Wahudumu wa afya kituo cha Bujunangoma wakimuaga aliyepona ugonjwa wa Marburg.

Ameongeza tena kuwa, “namshukuru Mungu ameniponyesha na watoaji wa huduma kwakweli nawashukuru sana wamenihudumia vizuri na leo naenda nyumbani wameniruhusu, sikutegemea kama naweza kurudi nyumbani.”

Mganga Mfawidhi wa hospital ya Bujunangoma Noel Saitoti ameeleza hali aliyokuwa nayo mgonjwa huyo alipoletwa kituoni hapo March 16 na mpaka sasa kuwa, “ni mgonjwa ambaye dalili zote zilikuwepo awali alikuwa na homa, anatapika na tumbo linamuuma kwahiyo alitengwa lakini sasa dalili zile zimekwisha ondoka kabisa na anaendelea vizuri mpaka kufikia hatua ya kumruhusu.”

Aliyepona Marburg akiwa na ndugu zake kwenye makaburi walipozikwa wanafamilia waliokufa kwa ugonjwa huo.

Naye afisa ustawi wa jamii – Mkoa wa Kagera Rebeka Gwambassa ameelezea jinsi walivyofurahia kwa kumfikisha nyumbani mtu huyo akiwa na afya nzuri na anaendelea vizuri huku mtu huyo ambaye alikuwa mgonjwa waMarburg, akitembelea makaburi walipozikwa ndugu zake watatu, akiwemo mama yake waliofariki dunia kutokana na ugonjwa Marburg.

Miundombinu barabara za utalii Kilimanjaro yaimarishwa
Mikataba ya Bilioni 284.14 yasainiwa ujenzi Skimu za umwagiliaji