Mshambuliaji na Kinara wa mabao wa Klabu ya Young Africans Fiston Kalala Mayele, amesema licha ya kikosi cha klabu hiyo kukabiliwa na mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Geita Gold FC, amesema akili na hesabu zake ni kutetema dhidi ya Simba SC Aprili 16, mwaka huu.

Mayele ambaye mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Simba SC alishindwa kuziona nyavu, hivyo kukosa fursa ya kushangilia kwa staili yake ya kutetema, amesema mchezo wao dhidi ya Simba SC utakuwa mgumu jambo ambalo linamfanya kuwa na kazi ya ziada ya ili kutimiza azma yake hiyo.

Mshambuliaji huyo kutoka DR Congo amesema kwa sasa anauwazia mchezo huo licha ya kwamba michezo iliyopo mbele yao ni dhidi ya Geita Gold kwenye Kombe la ASFC na kisha Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu kabla ya kuivaa Simba SC.

“Mchezo wa Simba SC na Young Africans huwa mgumu, nitahakikisha napambana kuipa ushindi timu yangu kwenye mchezo huo nikishirikiana na wachezaji wenzangu.”

“Ninataka nimalize msimu huu nikiwa nimeifunga Simba, naamini hakuna kitakachoshindikana ukiwa na malengo,” amesema Mayele.

Amesema anashukuru ushirikiano wanaopewa na mashabiki wao kwenye kila mchezo wanaoucheza ukiwamo ule wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika uliomalizika hivi karibuni dhidi ya TP Mazembe, Lubumbashi nchini DR Congo.

Mayele amesema wanaingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Geita Gold, watakaoucheza Jumamosi (April 08), ukifuatiwa na wa Ligi Kuu ambao watakutana na Kagera Sugar (Aprili 11), kabla ya kukutana na watani wao, Simba SC.

Rais UEFA azugumzia kashfa ya Waamuzi, Barca
Trilioni 8.64 kuendeleza miradi saba ya vipaumbele nchini