Idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi watalii milioni 2.4 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 199.5.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hii leo Aprili 5, 2023 wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024 bungeni jijini Dodoma.
Amesema, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeendelea kuwa hifadhi bora duniani ambapo kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2022 imepata tuzo ya dhahabu ya utoaji wa huduma bora iliyotolewa na European Society for Quality Research.
Majaliwa ameongeza kuwa, Serikali imeendelea kuimarisha sekta za maliasili na utalii kupitia utekelezaji wa programu mbalimbali ili kukuza utalii, kuitangaza nchi yetu na vivutio vyake kitaifa na kimataifa pamoja na kuimarisha mchango wa sekta hizo kwenye pato la Taifa.
Amesema katika mwaka 2022/2023, programu mbalimbali zimeendelea kutekelezwa ikiwemo Programu ya Tanzania – The Royal Tour na utangazaji wa vivutio vya utalii kupitia matukio mbalimbali na vyombo vya habari ikiwemo Tanzania Safari Channel.
Aidha, Majaliwa amesema kutokana na jitihada hizo, idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kutoka watalii 922,692 katika mwaka 2021 hadi kufikia watalii takriban milioni 1.4 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 57.7.