Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wamejivunia kuwa na msimu bora zaidi kuwahi kutokea kwenye historia ya klabu hiyo kutokana na mafanikio makubwa walioyapata na inayoendelea kuyapata kwenye michuano yote inayocheza hadi sasa.

Afisa Habari wa klabu hiyo, Ally Kamwe amesema Young Africans ipo kwenye asilimia nyingi za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini wanalitafuta Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, lakini pia wametinga Hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

“Msimu huu umekuwa wa mafanikio kwetu na tumeweka rekodi mbalimbali, kwanza tumekuwa timu ya kwanza Tanzania kuifunga TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Pia tumekuwa moja ya timu tatu ambazo zimeifunga TP Mazembe nyumbani na ugenini,” amesema.

Ameongeza: “Timu hizo ni sisi wenyewe Young Africans, US Monasrtir ya Tunisia msimu huu na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini misimu kadhaa nyumba, zaidi ha hapo hakuna timu yoyote Afrika iliyowahi kufanya hivyo.”

Wakati Young Africans ikiweka rekodi hiyo, Kamwe amesema mafanikio iliyoyapata ni kwamba mpaka sasa wapo kwenye michuano mitatu na wanafanya vema.

“Sisi ni mabingwa watetezi na msimu huu tunaendelea kuongoza ligi na tuna asilimia kubwa ya kulichukua taji la Ligi Kuu na lengo ni kuchukua yote pamoja na Kombe la ASFC.

Kumbuka huku kwenye ASFC tupo hatua ya Robo Fainali na tunakwenda kucheza Jumamosi dhidi ya Geita Gold, tunajua siyo mechi nyepesi kwa sababu timu hiyo ina kocha mzuri na wachezaji wake wana viwango vikubwa.

“Lakini sisi lengo letu kama nilivyosema msimu huu ni wa mafanikio ya kuchukua Ubingwa wa Tanzania Bara, Kombe la ASFC, halafu tupo kwenye Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huko nako tunataka kufanya vizuri,” amesema Kamwe.

Msimu huu Young Africans imetolewa kwenye michuani miwili tu kati ya mitano ambayo imeshiriki ambayo ni Kombe la Mapinduzi na Ligi ya Mabingwa Afrika ilipoodolewa kwa jumla ya mabao 2-1 na Al Hilal ya Sudan na kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho ambapo ilifanikiwa kuiondoa Club Africain ya Tunisia kwenye hatua ya mchujo, kabla ya kutinga hatua ya makundi na sasa Robo Fainali.

Lukaku azua kasheshe Italia, wamarekani wachachamaa
Haipendezi kuona wanaojitolea wanakosa sifa za kuajiriwa